Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian ametoa onyo kwa wafanyabiashara wanaoingia mkataba na wakulima wa mwani kununua zao, kisha kutowalipa fedha kwa wakati kuacha mara moja tabia hiyo.
Akizungumza Leo Juni 15, 2025 wakati wa uzinduzi wa kambi ya mafunzo ya ukuzaji stadi za ujasiriamali na ujuzi wa ndani katika uchumi wa buluu kwa vikundi 12 vya wanawake na vijana kutoka mkoani Tanga na Pemba, amesema wakulima wa mazao ya bahari hawana soko la uhakika wala vifaa, hivyo hawastahili kutapeliwa badala yake wanufaike.
“Wanaowatapeli wakulima wa mwani kwa kisingizio cha kuingia mikataba ya ununuzi waache mara moja,”amesema.
Kiongozi wa mradi wa Resea unaosimamia mafunzo hayo, Perpetua Angima amesema lengo lao ni kuwajengea wanawake na vijana ujuzi wa ndani na ujasiriamali kama kupanga mpango wa biashara, kufanya tathimini ya kimkakati ya biashara, maandalizi ya uwekezaji na masoko kwa mazao ya bahari.
Mwakilishi wa Umoja wa Kimataifa wa Kulinda Uasili, Dk Elinasi Monga amesema changamoto waliyobaini wanawake na vijana wengi katika sekta ya bahari ni ukosefu wa stadi za kupanga na kuendesha biashara, uelewa mdogo wa mnyororo wa thamani endelevu, ukosefu wa zana za kuvutia mitaji na maandalizi madogo ya uwekezaji na ujuzi wa ndani.
Saada Salehe Ali kutoka wilaya ya Wete Pemba na Mohamedi Zuberi wa wilaya ya Mkinga Tanga kwa nyakati tofauti wameonyesha matumaini yao kwa kupata mafunzo hayo, wakieleza kuwa wanatarajia kupata manufaa zaidi hasa kwenye suala la kuboresha bidhaa zao na kutafuta soko la mazao bahari.
Serikali kwa kushirikiana na Mradi wa ReSea unaotekelezwa na Mission Inclusion, IUCN, WFT-T na Ocean Hub Afrika kwa msaada wa Serikali ya Canada wameandaa mafunzo hayo ili kuwapa wanawake na vijana nafasi ya kujifunza jinsi ya kukuza biashara zao za uchumi wa buluu.
Imeandikwa na Rajabu Athumani …...more
...more
Show less